Mwanangu nakuandikia makala hii kukukumbusha kuwa maisha yamebadilika, mwanangu unaweza ikawa unajiuliza maisha yamebadilika katika nyanja ipi! Lakini mwanangu hii ni kwa ajili yako wewe na jamii inayokuzunguka.

Mwanangu najua unakumbuka kile kikao tulichokaa pamoja na mama yako tukikuasa kuhusu kumshika huyo elimu na kukuhimiza kuwa usimwache aende zake.

Elimu umemshika, umesoma mpaka sasa umepata pHd, ya mambo ya biashara! Hongera sana mwanangu! Kitu pekee ninachotaka kukukumbusha leo ni kuwa anza kufatilia elimu ya kubadilisha pHd kuwa ugali.

Maisha yamebadilika sana ukilinganisha na kipindi chetu, tulisafiri kilomita nyingi kuangalia fursa tena pasipo na mawasiliano ya sehemu unakokwenda! Wewe mwanangu unapata bahati ya kuwasiliana mpaka nchi za mbali ukiwa chumbani, jaribu kufikiria kwa kina juu ya fursa hii na uifanye kwa hali zote!

Mwanangu usiwe miongoni mwa wanaolalamika mtaani, toka na uanze kubadilisha pHd kuwa mkate!

Tukutane kesho mwanangu naamini barua hii utaipata!