Anaandika Dady Lutelemla
NGUVU YA UJINGA
_________________________________________
Wahenga wanasema “ni heri ukose nguvu lakini upate akili”. Wenye akili huwatumia wenye nguvu kufikia malengo yao kuliko kinyume chake (wenye nguvu kuwatumia wenye akili).
Hata hivyo uko ukweli mwingine mchungu katika maisha. Ni ule wa kwamba “ujinga ni mtaji” na wajinga wakiungana ni hatari kwa jamii nzima.
Kwa nini ujinga una nguvu na kuwa mtaji? Kwa nini umoja wa wajinga una nguvu kuliko hata umoja wa wenye akili?
Kwanza, WAJINGA NI WENGI. Wingi wa wajinga una nguvu kuliko usahihi wa wenye akili. Kwa hiyo wajinga wengi wakiungana kupinga kitu au kuunga mkono kitu, kitafanikiwa hata kama mafanikio hayo yana maana ya kuwatesa wajinga hao wenyewe walio wengi. Kwa ujinga wao, wanaweza kuungana kuunga mkono mpango wa kuwaua wajinga wote na ukafanikiwa. Adui mkubwa wa wenye akili, wenye madaraka na matajiri kote duniani ni watu wajinga.
Pili, silaha ya wenye madaraka dhidi ya watu wajinga ni matumizi ya nguvu. Elimu ni adui wa ujinga na wajinga huwa hawapendi kutumia dawa hii. Kwa hiyo, wenye akili na madaraka hupenda kutumia nguvu kuwatawala wajinga kuliko kutumia akili.
Yaweza kuwa salama kwa mtu kuzungukwa na maadui zako au wapinzani wako kuliko kuzungukwa na wajinga. Katika kukulinda, wajinga wanaweza kukuua wakidhani wanakulinda.
Msikwazike, ujinga siyo tusi. Ni hali mpito inayoweza kuondoka.
0 Comments