Watu wengi wanakata tamaa pale wanapoanzisha kitu na kushindwa. Wengi wanaposhindwa wanaona huo ndio mwisho wa wao kufanya kitu kikafanikiwa. Wanaona kama mafanikio ni ya watu wachache tu na wao sio bahati yao kufanikiwa, kitu ambacho naamini hakina ukweli wowote.

Mafanikio sio ya watu wachache tu. Kila mtu anaweza kufanikiwa kama akifanya,akiwaza na kujituma kama watu waliofanikiwa. Kushindwa sio mwisho wa maisha, sio mwisho wa safari yako ya mafanikio.

Kama umeshindwa hauko peke yako. Ukweli ni kwamba watu wote unaowaona wamefanikiwa leo, kwa namna moja au nyingine kuna sehemu kwenye maisha yao walishindwa. Tena wengine walishindwa zaidi ya mara moja, lakini hawakukata tamaa, waliendelea kujaribu mpaka walipoona matokeo.

Umeshindwa mara moja tu na unataka kukata tamaa? Nani amekwambia kwamba biashara ni rahisi kwamba ukijaribu mara moja tu utapata matokeo? Nani aliyekwambia kwamba hamna kushindwa? Nani aliyekwambia? 

Unaposhindwa ni njia nzuri ya kujifunza na kujaribu tena kwa nguvu mpya na hamasa mpya na sio kukata tamaa. Moja ya msamiati ambao unatakiwa kufuta kwenye maneno yako ni ‘kukata tamaa’. Yaani ilo neno lifute kabisa kwenye maneno yako.

Usikate tamaa unaposhindwa. Jifunze kwa kushindwa kwako kwa kuangalia ni wapi ulikosea na jaribu tena  na tena na tena mpaka uone matokeo. 

Kama kuna mtu alikwambia kwamba hakuna kushindwa kwenye safari ya mafanikio basi alikudanganya. Kushindwa kupo. Lakini unaposhindwa lazima ujifunze kitu, hakuna maana ya kushindwa alafu ukajaribu kufanya tena kwa njia zilezile, ukifanya hivyo utaendelea kushindwa tu. 

Unaposhindwa jifunze kitu na jaribu tena mpaka uone matokeo. Kushindwa sio mwisho wa kujaribu tena.
Tafakari njema rafiki yangu.

Hamasa Jukwaani> Dady Lutelemla >+255620306815