Kijana Wangu; Ndoa hujengwa kwa mawe ya upendo na sakafu ya utii! Kupenda ni jukumu la mwanaume. Kutii ni jukumu la mwanamke. Ukimpenda atakutii. Ukimchukia atakudharau. Kumpenda mwanamke ni kumhudumia. Hatupendi kwa mabusu na tabasamu. Tunapenda kwa fedha na dhahabu! Mabusu na tabasamu ni vionjo vya mapenzi, siyo mapenzi.


Kijana Wangu; Ukishindwa kumhudumia mwanamke atajihudumia. Akijihudumia atakudharau. Hujawahi kusikia wanasema siweza kukaa na mwanaume asiyenihudumia? Na hii siyo kwa wanawake tu. Ni sehemu zote. Duniani hajawahi kuheshimiwa mtu. Yanaheshimiwa matokeo ya mtu. 


Huna cheo nani atakutii? Huna umaarufu nani atakutii? Huna pesa nani atakutii? Huna pesa hata mbwa wako anaweza kukuuma!


Kijana Wangu; Tusiwapuuze sana waliosema hapendwi mtu, inapendwa pesa. Kuna jamaa moja linawafundisha wanawake huko mitandaoni kwamba cha peke yako ni kaburi tu. Mafundisho mengine ni ya hovyo sana lakini tutafanyaje sasa. 

 

Kijana Wangu; Uanaume ni kubeba majukumu ya nyumba ndiyo maana ukaitwa baba mwenye nyumba. Ni gharama kuitwa baba mwenye nyumba! Kiburi cha mwanamke ndani ya nyumba ni matokeo ya baba mwenye nyumba kushindwa kuibeba nyumba yake.


Kijana Wangu; Mwanamke yuko open. Mnamfuata wenyewe. Habembelezi kuolewa. Wewe ndio ulimbembeleza. Tena ulijitutumua hadi akakukubali wewe na kuwapiga chini wanaume wote waliomfukuzia. Ukajiona kidume. Basi mantain udume hadi kwenye nyumba.


Kama uliazima suruali na saa ya mkononi kumpata basi lipa gharama za uongo. Mwanamke hanaga utani. Ukishindwa kumhudumia usilalamike ati hakuheshimu. Naomba unielewe. Usiwe mbishi kama mawe ya baharini, yanapigwa na mawimbi kila siku lakini hayatakati.  


Kijana Wangu; Mwanaume wa shoka hawezi kulialia kwamba mke wake anamdharau. Hivi mkeo anashindwa vipi kukutii kwa mfano? Hebu jitathmini kama unatosha kwenye hiyo nafasi. 


Kijana Wangu; Pesa huna halafu unataka uheshimike. Hakuna heshima kwenye hamna. Uvumilivu kwenye hamna una ukomo. Filisika tujue tabia ya mkeo.Iko hivyo! Ni fedheha lakini ndio basi tena.


Kijana Wangu; Unataka mwanamke wa hadhi ya juu, akikuomba elfu hamsini unazima simu! Si bora ukajitafutie mwanamke wa hadhi yako ukimnunulia karanga za kuchemsha na bando ya jero anakupa vyote mwili na roho badala ya kukuua kwa stress? 


Ya nini kujipunguzia siku za kuishi kwa kung’ang’ani vilivyo nje ya uwezo wako? Yani nini??? Nauliza kwa sauti ya Steve Nyrere! Ya nini mie!!! Haya mambo ya kung’ang’ania mavitu ya gharama msizoziweza ndo utasikia presha imepanda, figo zimefeli, unakufa.   


Kijana Wangu; Ndoto ya kila mwanamke ni kupata mwanaume wa kumdekeza na kumlinda.Hii ni kwa wanawake wote wenye pesa na malofa. Ukiyaweza hayo atakutii hadi utafikiri ni spy kumbe mkeo wako. 


Akiona hueleweki, atasimama mwenyewe kujihudumia na hapo usishangae akiianza kukutuma. Mr. Mushi, washa moto nimepita sokoni kununua mboga. Ukiishiwa mkeo anaanza kukuita kwa jina la ukoo.


Kijana Wangu; Hutaki kutumwa chacharika. Ukikaa nyumbani utatumwa! Ukitumwa usilalamike ati mkeo anakupanda kichwani.


Kijana Wangu; Unamlazimisha mwanamke akusaidie kutafuta pesa; akikwambia na wewe umsaidie kupika unasema amekupanda kichwani; kupika siyo jukumu lako; kwani na yeye kutafuta pesa ni jukumu lake? Ukiona malumbano kama hayo kwenye ndoa tambua ndoa imekushinda, rudi nyumbani ukajipange upya.  


Vinginevyo utaanza kuchepuka hovyo na kusema mkeo ndio kakusababishia uchepuke. Bure kabisa! Nimewahi kusikia majibu ya namna hii pia kwa wanawake washenzi. Kwamba wame zao ndio chanzo cha kuchepuka na wakati ni tabia zao tu. 


Ndo yale yale kwamba mwanaume anaweza akamsaliti mke na bado akawa anampenda lakini mwanamke akimsaliti mume wake hampendi. Usaliti ni usaliti tu.


Kijana Wangu; Jijengee mazingira ya mkeo kukuheshimu usije kuwa msaliti. Fanya kazi yoyote ile hata kuzibua vyoo usikae idle.Ukikaa idle atakuchoka. Mke akikuchoka hata ukijamba utasikia; Baba Neema ushajamba hivyo!  


Kijana Wangu; Kama pochi halitoshi hata umtishie vipi dharau ziko palepale. Jikeep busy kabla mke hajakukeep busy ukakimbia nyumba yako. Ila usiwe busy for nothing kama nzi. Jikeep busy kama nyuki. 


Nyuki na nzi wote wako busy, kila sehemu utawakuta wakirukaruka na kutua kuanzia chooni hadi kwenye maua na vidonda; tofauti zao utaziona mwisho wa siku, mmoja ataleta asali, mwingine atakuja mikono mitupu.


Uaminifu huna! Pesa huna. Halafu unataka ndoa. Unataka kufa? Kijana Wangu bana. Wanawake siku hizi wanakwambia, "ni bora nikalilie ndani ya gari kuliko kulilia juu ya baiskeli," kakiwa na maana kwamba wanaume wote ni wahuni; hivyo ni bora aende kwa muhuni mwenye hela atapotezewa muda lakini ataambulia chochote kuliko kwenda kwa muhuni maskini atapotezewa muda na kutoka kapa! Vijana wangu duniani mnayo dhiki, jipeni moyo mtashinda!


Kijana Wangu; Tafuta pesa upate heshima. Hakuna jinsia iliyokuja duniani kuteseka kwa ajili ya jinsia nyingine! Hilo siyo lengo la ndoa! Kama ndilo basi ndoa siyo mpango wa Mungu! Huo ni mpango wa shetani!


Kijana Wangu; Kuna watu wanadhani ndoa ni kama ufalme wa mbinguni kwamba kuingia lazima umpate mkamilifu wa kuingia naye. Hakuna kitu kama hicho! Kila binadamu ana kilema chake, mkamilifu ni Mungu tu. 


Habari za kusema huwezi kuoa mwanamke asiyejua kupika ni ukorofi! Hivi na wanawake wakisema hatuolewi na wanaume wasiojua kutafuta pesa itakuaje?Si kuna wanaume watakufa bila kuoa hapa duniani? 


Kijana Wangu; Unataka mwanamke anayejua kupika na wakati hujui kutafuta pesa. Atapika nini sasa? Au unataka akutafutie na vya kupika? Usitafute balaa. Kwa mara ya kwanza Adam alipoletewa chakula na mke wake walifukuzwa Eden!


Kijana Wangu; Ndoa ni mchezo wa pata potea. Ukiingia kwenye ndoa usitegemee kupata vyote. Lakini pia huwezi kukosa vyote pia. Tumia muda wako kuenjoy unachokipata kuliko kujutia usichokipata. Kama hakipo hakipo tu. Kwa nini kikunyime usingizi? 


Kijana Wangu; Msilazimishe kupata wanawake wakamilifu ambao hawapo hapa duniani labda muwaumbe wenyewe. Ukiingia kwenye ndoa kuna haki lazima uzipoteze. Haki ya kuishi kama mvulana ndani ya ndoa itapotea; maisha ya kula gengeni na kuangalia mpira hadi asubuhi.utayakosa. 


Ukiona bado una hamu ya kuishi kivulana omba talaka urudi kwa mama yako.Utajitahidi kuficha lakini za mwizi ni arobani.


Kijana Wangu; Huna sifa hata moja ya kuwa mume bora lakini unatafuta mwanamke mwenye sifa za kuwa mke bora! Atoke wapi. Mungu humpa kila mtu wa kufanana naye; yaani mshenzi na mshenzi mwenzake; muungwana na muungwana mwenzake!


Kijana Wangu; Nyumba yenye upendo na utii haikosi bahati. Nyumba yenye chuki na dharau haikosi mkosi! Kajenge nyumba yenye upendo na utii na Mungu atakubariki.

Leo katika Jukwaa la fikra tumebarikiwa na mwandishi nguli. Mwl.Denis Mpagaze

Muhenga wa Karne ya 21!