Leo naomba tujifunze tabia za watoto ambazo tunaweza kujifunza na kuzitumia katika safari yetu ya mafanikio. Tulipokuwa watoto tulikuwa na tabia nyingi nzuri, lakini kadiri tunavyokuwa tabia hizi tunazipoteza.

Tabia hizi upotea kutokana na mazingira tunayokutana nayo baada ya kuzaliwa. Familia na jamii tunayokutana nayo ni moja ya sababu ya tabia hizi kupotea. Lakini pia vyombo vya habari, mitandao ya intaneti na tekinolojia ni sababu nyingine ya kupotea kwa tabia hizi.

Tabia hizi zinapopotea, zinatufanya tuishi maisha ya kawaida kutokana na misimamo na imani iliyopo kwenye jamii zetu. Tunalidhika na maisha na kuishi kama wazazi au jamii yetu inavyoishi. Ndoto kubwa tulizokuwa nazo utotoni tunaziweka pembeni kwa sababu watu na mazingira yanayotuzunguka yanatuambia kwamba haiwezekani. Na cha ajabu  tunashindwa kujiamini na tunawaamini watu au mazingira yanayotuzunguka. 

Ndoto tulizokuwa nazo zinakufa. Mawazo tuliyokuwa nayo yanakufa. Tunakubaliana na mazingira na jamii inayotuzunguka. Na sisi tunaanza kuona kwamba haiwezekani kama jamii inavyo ona. Tunaamini maisha ndivyo yalivyo na tunaendelea kuishi kama jamii zetu zinavyoishi.

Hizi hapa ni tabia nne walizonazo watoto tunazoweza kujifunza na kuzitumia katika mafanikio yetu;

1). Ujasiri.

Kipindi tukiwa watoto, wazazi wetu walituambia hiki au kile kitu ni kibaya na walitukanya tusifanye. Wazazi walituambia moto ni mbaya na tukiugusa utatuunguza. Wazazi walituambia mambo mengi ya kuepuka ambayo waliona ni mabaya. Na hicho ni kitu kizuri, kwa sababu walionyesha upendo wao kwetu, na kuna kipindi walikuwa tayari kutuchapa pale tunapoenda kinyume na yale wanayo twambia.

Kwa nini nasema mtoto ni jasiri. Nasema hivi kwa sababu, ijapokuwa wazazi na jamii ilituambia vitu fulani ni vibaya tusifanye lakini mara nyingi tulikuwa tunafanya. Tuliambiwa moto ni mbaya lakini tuliushika kwa sababu tulitaka kujionea na kuthibitisha wenyewe. Kupitia kufanya hivi vitu ambavyo wazazi wetu walitwambia ni vibaya ndio tulijifunza vizuri zaidi kwa sababu tulithibisha na kujionea wenyewe.

Hii tabia ya ujasiri inakufa kadiri tunavyokuwa wakubwa. Tunaogopa kujaribu vitu ambavyo tunaambiwa na jamii au wazazi wetu kwamba ni vibaya. Tunapotaka kufanya kitu kwa ajili ya ndoto zetu, ujasiri unapotea kwa sababu tumeambiwa kwamba haiwezekani. 

Mawazo ya biashara tuliyokuwa nayo yanakufa. Ndoto kubwa tulizokuwa  nazo zinakufa. Ujasiri wa kujaribu ili tuthibitishe wenyewe unakufa. Tunakubaliana na jamii na tunaishi maisha ya kawaida kama wengine au jamii inavyotaka.

Rafiki kama unataka kufanikiwa lazima huwe na ujasiri. Bila kuwa jasiri, itakuwa ngmu sana kwako kufanikiwa. Tabia hii ya ujasiri inatakiwa sana katika safari yetu ya mafanikio. Tujifunze kwa watoto kuwa na ujasiri wa kujaribu hata kama jamii inatwambia haiwezekani.

2). Kufurahi na kuishi leo.

Watoto muda mwingi wana furaha. Hata kama kuna kitu kibaya kimetokea, mtoto atatumia muda mchache kulia na baada ya hapo utamukuta ni mwenye furaha tena. Mtoto akiwa mikononi mwa mama yake, hata hawazi kesho itakuwaje. Yeye anachojua ni kuishi na kufurahi leo, sio kesho. Nguvu zake zote anaziweka leo na sio kesho. Tabia hii ya kuishi leo na sio kesho inawafanya watoto kuwa na furaha hata kama hawajui kesho kutatokea nini. 

Tukiwa watu wazima mambo yanabadilika, tunawaza sana kesho itakuwaje. Tunaingalia sana kesho na sio leo. Tunasema kesho nitaanza kufurahi baada ya kupata kitu fulani.

Rafiki furaha ni leo sio kesho. Kufurahi sio mpaka kesho au mpaka upate kitu fulani. Fanya vitu ambavyo vitakufanya huwe na furaha sasa sio kesho. Furahia safari yako ya mafanikio. 

Lakini pia tunapopita kwenye majaribu au changamoto, huwa inatuchukua muda mwingi mpaka turudie hali yetu ya kawaida, kinyume na mtototo ambaye inamchukua muda kidogo tu. 

Tujifunze kwa watoto kwamba tunapopita katika kipindi kigumu, sio kipindi cha kulalamika na kubaki kwenye hali ya kuumia kila siku. Kipindi kama hicho ni wakati  mzuri wa kuangalia wapi umekosea na kujifunza na uendelee mbele. Usibaki kwenye maumivu kwa muda mwingi kwa sababu maisha ni mafupi sana rafiki yangu, jifunze na endelea mbele.

Kuishi ni leo na sio kesho rafiki yangu. Mamabo unayofanya leo ndo yanaonyesha utakuwa wapi kesho.Mafanikio ni muunganiko wa vitu vidogovidogo unavyofanya kila siku. Kama unataka kufanikiwa kuwa na mpango wa kufanya kitu kila siku na sio kusema utafanya kesho.

3). Kusamehe na Kusahau.

Mototo ni mwepesi sana kusamehe na kusahau. Ukimchapa mtoto, atalia kwa kipindi kifupi na baada ya hapo ataendelea na michezo yake kama kawaida, utazani hakuna kitu kilichotokea. 

Tujifunze kusamehe na kusau hata kama watu wametuumiza. Kusamehe na kusaua ni kwa ajili yetu na sio yule tunaye msamehe. Najua kuna wakati inakuwa ngumu sana kusamehe, hasa pale watu wanapotuumiza, lakini rafiki jifunze kusamehe kama unataka kufanikiwa. 

Ukisamehe unakuwa na amani na furaha ya kuendelea na safari yako ya mafanikio. Usiposamehe unabaki na uchungu moyoni, unaoweza kukuzuia usifanikiwe na ukose furaha. Samehe kwa sababu unataka kuwa na amani na furaha. 

4). Kujaribu tena baada ya kushindwa.

Kama tusingejaribu kutambaa tukiwa watoto basi tusingeweza kutambaa. Kama tusingejaribu kusimama, basi tusingeweza kusimama. Kama tusingejaribu kutembea wakati wa utoto, basi tusingekuwa tunatembea sasa. 

Utakubaliana na mimi kwamba hatukutembea siku ya kwanza tu tulipojaribu kutembea, tulitembea kwa sababu tulijaribu mara nyingi kadiri tulivyoweza. 

Kama unajua kuendesha baiskeli, unakumbuka ni mara ngapi ulijaribu kabla ujaweza? Nina uwakika ni zaidi ya mara mbili. 

Sasa sijui kwa nini tunapokuwa watu wazima tunataka tukifanya kitu tupate matokeo ya haraka, tunataka tukifanya kitu leo, kesho tupate matokeo. Tunataka tukifanya kitu mara moja tupate matokeo. Tukishindwa mara moja au mbili tunakata tamaa ya kuendelee tena. Tunashindwa kujaribu tena.

Rafiki kama una uwakika kwamba kitu fulani ndio dhumuni lako au ndio kitu unachotaka, basi jaribu mpaka uweze. Jaribu , jaribu, jaribu, usikate tamaa mpaka uone matokeo.

Karibu jukwaani