Kila mtu anapenda kuwa na maisha mazuri. Kila mtu anapenda awe na uhuru wa kifedha. Tunajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili tupate uhuru wa kifedha. Ili tuishi vizuri, tunahitaji fedha. Kwa dunia ya sasa, usipokuwa na pesa ya kukutosha maisha yatakuwa magumu sana kwako.

Ingawa watu wengi tunapenda kuwa na pesa za kututosha, lakini bado uhuru wa kifedha umekuwa ni changamoto kwetu. Leo nakushirikisha mambo matatu ambayo ukiyafanya yatakupeleka kwenye uhuru wa kifedha. Haya hapa ni mambo matatu ya kufanya kama unataka kuwa na uhuru wa kifedha;

Elimu ya fedha.

Watu wengi hatuna elimu ya fedha. Watu wengi wanapopata pesa wanaitumia vibaya. Bajeti kwa wengi ni changamoto. Ni asilimia chache sana ya watu, Tanzania wenye elimu ya fedha. Tunasoma maisha yetu yote kuanzia shule ya msingi mpaka chuo bila kufundishwa elimu hii.

Rafiki yangu ili utuke hapo ulipo na kufikia uhuru wa kifedha, ni lazima ujifunze kuhusu fedha. Fedha ni kama fani zingine, kuna ujuzi unatakiwa kuwa nao ili uweze kuitawala fedha. Uhuru wa fedha unakuja kwa wewe kuwa na ujuzi (elimu) sahihi wa fedha.

Kwa sababu wengi wetu hatujafundishwa elimu hii, ni jukumu letu kujifunza. Tafuta semina za fedha ujifunze. Sikiliza kanda, CDs, DVDs zinazozungumzia pesa. Soma vitabu vinavyozungumzia fedha ili kuinoa akili yako kuwa na elimu au ujuzi kuhusu fedha.

Kuweka akiba.

Kuna msemo wa Kiswahili unasema ‘ akiba haiozi’. Kama ulikuwa hauna tabia ya kuweka akiba, nakushauri anza leo kuweka akiba kwa kila fedha unayoingiza. Jilipe kwanza kwa kuweka angalua asilimia kumi ya kipata chako kama akiba na hakikisha hutumii fedha hiyo kwa matumuzi mengine zaidi ya kuwekeza.

Tatizo sio kiasi cha pesa ulichonacho. Anza kujinyima na kuweka akiba hata kama unapata kiasi kidogo. Itakuwa ngumu mwanzoni, lakini kadiri unavyofanya kila unapopata pesa, hii inageuka na kuwa tabia yako na utashangaa kila unapopata pesa unaweka akiba bila kujiuliza mara mbilimbili, kwa kingereza wanasema inakuwa ‘ automatically’.

Pesa hii hakikisha unaitenga na kuiwekeza. Unaweza kuwekeza kwenye vipande, hisa au amana za benki. Lakini pia unaweza kuwekeza kwenye ardhi na majengo. Kabla ya kuwekeza hakikisha unakuwa na elimu sahihi na sehemu unayoenda kuwekeza.

Nidhamu ya fedha.

Elimu nzuri ya fedha bila kuwa na nidhamu ni bure. Hakuna maana kuwa na elimu nzuri ya fedha na ukaanza kuweka akiba na baada ya muda ukarudia maisha yako yaleyale ya mwanzo.

Nidhamu ni muhimu sana. Uhuru wa kifedha unahitaji nidhamu binafsi ya fedha. Unahitaji kuwa na nidhamu kwenye matumizi yako, nidhamu ya kujilipa kwanza, kuweka akiba na kuwekeza, na nidhamu ya kuendelea kujifunza kuhusu elimu ya fedha. Elimu haina mwisho na mambo yanabadilika kila siku, lazima uendelee kujifunza kila mara ili kuendana na kasi ya dunia.

Unaweza kabisa kuwa tajiri(uhuru wa fedha) kama utajifunza elimu ya fedha, utajifunza kuweka akiba na kuwekeza, na kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha.

Elimu. Akiba. Wekeza. Nidhamu.

Karibu Jukwaani!

Wako Dady Lutelemla >0620306815