Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.” Mithali 10 :19

Kuna watu tunapenda sana kuongea. Wapo watu wakikaa sehemu bila kusema hata neno moja wanajisikia kuumwa. Kila kitu tunajifanya tunajua, kila mada ikisemwa tunadakia bila hata ya kujua tunaongea nini.

Neno la Mungu linatuonya kuongeaongea sana bila mipango. Kwenye maneno mengi lazima uovu utakuepo, lazima kuna uongo tu utakuepo ndani, lazima kuna maneno ambayo hayana maana utayaongea tu.

Bora kunyamaza, kuliko kuongea ukasema yasiyo na maana. Kuongea vitu visivyo na maana vitashusha heshima yako mbele za watu. Ukikaa kimya utalinda heshima yako. Neno la Mungu linasema “ Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili”. Kuzuia midomo yako kuongea vitu visivyo na maana ni akili mbele za Mungu.

Mtu anayezuia mdomo wake kuongea mambo yasiyo na maana au maovu, Biblia inamuita mtu huyo kuwa ni mtu aliye na akili. Ukipenda kuongeaongea sana lazima kuna sehemu utakosea tu. Ulimi ni kiungo kidogo lakini kinaweza kukufanya ukapotea kabisa. Sio kutenda dhambi tu lakini hata kujifunga wewe mwenyewe kwenye maisha yako.

Moja ya kitu unachotakiwa kuwa mwangalifu rafiki yangu ni ulimi wako. Chunga sana maneno unayosema. Sio kila kitu lazima uchangie au uongee, kuna vitu vingine ni hekima kabisa kukaa kimya. Kwani kuna kitu gani kitapungua kwenye maisha yako ukikaa kimya? Utapungukiwa na nini? Si bora ukakaa kimya kuliko kuongea sana na ukasema maovu, ukasema mambo yasiyo na maana.

Ulimi huu usipoutumia vizuri utakufanya ukosane na Mungu na watu. Watu wanaweza kukuchukia kwa sababu ya kuongeaongea sana. Chunga sana unachosema. Kama unaona jambo sio muhimu wewe kulisema sio vibaya ukanyamza kimya, ina faida mara mia kuliko kusema kitu kikakufunga wewe mwenyewe.

Sio kila kitu kwenye maisha yako unatakiwa kumwambia kila mtu. Kwa kuwa umefanikiwa kidogo, yaani kila mtu unataka ajue umefanikiwa. Kila mtu unamwambia. Angalia sana, kuna wengine japokuwa hawakwambii, lakini wanakuonea wivu.

Moja ya njia ya kupunguza watu wengine wasikuonee wivu ni kuacha kuwaambia watu kila kitu chako. Yaani unamwaga kila siri rafiki yangu, hata za chumbani, looh. Hacha hiyo tabia. Mungu apendi, hata binadamu hawapendi sema wanashindwa tu kukwambia. Mimi nimekwambia kazi kwako kuchukua hatua.

Punguza kuongea maneno mengi, ongea maneno yenye umuhimu wewe kuongea. Kama ukitaka kuongea na ukajua kwamba hakuna maana yoyote ya wewe kuongea ni bora ukakaa kimya, utakuwa umetumia akili sana.

Kuwa mwangalifu na ulimi ndugu yangu. Ongea mambo ya muhimu tu na yasio muhimu nyamaza, nakuhahakishia utakuwa mwenye hekima na akili. Ni bora kunyamaza, kuliko kusema ujinga na uovu.

Panda jukwaani nami pamoja.

+255620306815