Wakikuona huwezi, waonyeshe unaweza. Fanya kama maharage mabovu.Kabla ya kupikwa mama aliyoyaona mabovu aliyatupa jalalani lakini mvua iliponyesha yaliota. Maharage hayo yangesikiliza maneno ya mama leo yasingeota.
Ndani ya maharage yaliyooza kuna nguvu ya uhai, ni suala la maharage yenyewe kuamua. Kadhalika ndani yako kuna nguvu ya uhai ni suala la wewe kuamua. Kilichoumbwa na Mungu kina nguvu ndani yake. Mungu habahatishi.
Ukiitwa dhaifu unakubali wewe ni dhaifu. Hili ni kosa kubwa sana. Ile kuzaliwa tu tayari wewe ni mshindi. Kumbuka mlitoka kwa baba yako mamilioni ya mbegu lakini wewe tu ndo uliwashinda wote kuwahi kufika kwenye tumbo la mama yako, mimba ikatungwa, miezi tisa ikakua ukazaliwa.
Usisubiri nguvu kutoka nje ikuamshe. Hiyo itakuua. Tumia nguvu iliyoko ndani yako kuota kama maharage yaliyooza! Hata yai likipasuliwa na nguvu kutoka nje hupati kifaranga. Utapata kifaranga yai likijipasua lenyewe kutokea ndani! Kama huamini vunja yai uone kama utapata kifaranga.
Kumbuka jinsi Mungu anavyokuona ni tofauti kabisa na watu wanavyokuona. Wakikuona umeoza, Mungu anakuona hai. Wakikuona maskini Mungu anakuona tajiri.Wakikuona wa nini Mungu anakuona wa neema.
Waliokusalimia kwa dharau ipo siku watakusalimia tena kwa dharau kama hautajitahidi. Fanya kujitahidi!
0 Comments