*Uongo Unasaidia Lakini ni Sumu: Hoja 9!*

Kama unavitabia vya uongouongo fanya kuviacha maana hatari ni kubwa kuliko ahueni uipatayo kwa kudanganya. Uzuri lazima utashikwa tu maana za mwizi ni 40. We sema ukweli tu hata kama panga liko shingoni. Sema tu. Ni kazi ngumu kuacha uongo hasa ukizingatia uongo ni tabia ya binadamu.

Mtaalamu wa mambo ya uongo Bi Pamela Meyer anasema kila mtu ni muongo ndiyo maana unapokutana naye ndani ya dakika tatu za mwanzo lazima akudanganye na wewe umdanganye. Mnadanganyana.

Kuna watu, tena wengi tu bila wazazi kudanganya wasingezaliwa; na wengine bila uongo wasingepanda cheo piga ua maana uwezo wao tunaujua.

Sijui kwa dini nyingine lakini kwa Ukristo, uongo umekatazwa kwa amri na mifano hai. Amri ya Tisa inasema usimshuhudie jirani yako uongo. Kumdanganya mwenzako ni sawa na kumtwanga nyundo na panga la kichwa na kumchoma mshale. Soma Methali 25:18. 

Anyway ngoja niweke hoja 9 kuhusu uongo!

Hoja ya 1

Uongo mmoja unatosha kutilia shaka kila ukweli utakaousema daima! Ni bora uniambie ukweli niumie nipone kuliko kuniambia uongo nifurahi nikaja kujua nikakuumiza. Sisikitiki kwa sababu umenidanganya; nasikitika kwa sababu sitakuamini tena! Ukweli huuma mara moja, uongo huuma mara zote. Niambie ukweli.

Hoja ya 2

Kusema uongo ni kazi rahisi sana ila kuulinda ni kazi ngumu sana maana ukiwa muongo inabidi ukumbuke kila unachodanganya. Sasa utakumbuka vingapi katika hii dunia iliyojaa wendawazimu? Hata mwanamke aliyetoka kucheat hupitia kuni msituni na kurudi nazo nyumbani mume asijue. Hii nayo ni sehemu ya kuulinda uongo!

Hoja ya Tatu

Huwezi kuwadanganya watu wote kwa wakati wote labda vichaa. Unapoamua kunidanganya ni dhahiri umeniona mjinga, sina akili. Yaani umeamua kunidharau! Sikiliza unapopanga kunidanganya hakikisha una uhakika siwezi kujua vinginevyo usithubutu.

Hoja ya Nne

Bora kofi linaloumiza kwenye shavu kuliko busu la uongo kwenye shavu langu. Habari za kunidanganya kwa tungo za kwamba uongo wa daktari ni nafuu ya mgonjwa, utaelewa kama mimi ni mgonjwa siku nikijua uongo wako! Uongo ni soo, we omba Mungu lisibume! Likibumaga halizimikagi!

Hoja ya Tano

Uongo ni njia nzuri  na ya haraka ya kuharibu mahusiano mazuri mliyoyajenga kwa taabu na kudumu kwa muda mrefu. Usikubali juhudi zako zikaharibika kizembe. Naongea kama utani, siku utakapotembea uchi ndo siku hiyo utakapokutana na mama mkwe!

Hoja ya Sita

Uongo unapanda ghorofa kwa lift, ukweli unapanda kwa ngazi! Mwisho wa siku vyote vitakutana ghorofani na hapo ndipo wahenga wanasema za mwizi ni 40. Hapo lazima kiumane, kama ni ndoa inaishia hapo, cheo kinaishia hapo, urafiki unaishia hapo! Kumbuka ukinya njiani huwezi kukwepa nzi wakati unarudi.

Hoja ya Saba

Uongo ni msaada wa leo wenye hasara kesho! Kama unaujua ukweli ni bora kujikalia kimya kuliko kudanganya! Wahenga wanakwambia ukweli wote ni mzuri ila siyo vizuri kuusema vinginevyo ukimaliza kuusema kimbia. Mbadala wa kusema ni kunyamaza siyo kudanganya. 

Hoja ya Nane

Usimuamini muonga hata kama anasema ukweli. Fisi ni fisi tu hata kama akipaka wanja bado tabia za ufisi kuzengea mkono wako udondoke autafune iko palepale. Sasa we endelea kumuamini siku akikutafuna mikono ndio utaelewa kumbe ni kweli hata Shetani alikuwa Beby! 

Hoja ya Tisa

Uongo ni jibu la muda kwa tatizo la kudumu. Ni sawa na panado, inatuliza maumivu haitibu maumivu! Kuna watu uongo umewasaidia kupata mke, mume, kazi, pesa na vitamu vingi ambavyo leo vimekuwa vichungu! Nayasema haya kwa sababu nayajua. Au natania ndugu zangu?

Karibu Katika Jukwaa la Fikra tujenge nchi na Mwl. Denis Mpagaze na PHsDp Dady Lutelemla.