Kasi za ndoa kung'ata watu inaendelea kushika kasi. Haipiti siku mtu hajang'atwa! Iwe wacha Mungu na wasiomcha, wenye pesa na wasionazo; wasomi na wasiosoma; viongozi na wasio viongozi; wote wanang'atwa tu. Zamani mke kuua mume na mume kuua mke ilikuwa habari kubwa. Siku hizi ni habari ya kawaida sana!
Mpango wa Mungu umekuwa mpango wa Shetani! Hatari. Unajua kwa nini? Kuna sehemu tunakosea sana. Ngoja nitaje walau makosa machache!
Kosa la Kwanza
Tunatumia muda mwingi kuandaa harusi badala ya ndoa! Harusi ya siku moja inaandaliwa kwa vikao vya mwaka mzima;ndoa ya maisha inaandaliwa kwa mafunzo ya wiki moja kanisani! Kwa nini mafunzo ya ndoa yasiende hata mwaka mzima? Hii itasaidia mtu kufanya maamuzo sahihi ya kuingia kwenye ndoa au aache. Siyo lazima kila mtu kuolewa, na wala siyo lazima kila mtu kuoa. Kwani Yesu alimuoa nani?
Kosa la Pili
Wakati Mwanamke anaingia kwenye ndoa na mipango ya kumtunza mama yake; Mwanaume anaingia kwenye ndoa na mipango ya kutunza nyumba ndogo!
Lugha ya siwezi kuacha mama ateseke ni nzuri lakini ni hatari sana kwa ustawi wa ndoa yenu. Kuna jamaa aliwahi kusema, ukitaka ndoa yenu iwe salama hakikisha mkeo na mama yake haziivi.
Lakini utamaduni wa kumiliki nyumba ndogo ni hatari zaidi kwa ustawi wa ndoa yenu kwa sababu nyumba ndogo haili matembele! Nimeona niyaseme haya kwa vijana wenye mpango wa kuingia kwenye ndoa maana vifo vitokanavyo na ndoa vinauma!
Kosa la Tatu
Hii lugha ya siwezi kutumia hela niliyojitafutia kwa akili zangu kwa ajili ya matumizi ya familia ni lugha hatari sana. Kwanza nidharau kwa Mungu aliyesema ndoa huwafanya muwe mwili mmoja. Sasa hii lugha ya akili zako inatoka wapi katika mwili mmoja? Achana na ushamba wa changu changu chako chetu! Vijana mkiingia msifanye hayo.
Kosa la Nne
Kabla ya kuingia kwenye ndoa tunapimwa ukimwi tu badala ya kupimwa vyote, ukimwi na akili; unaweza kujikuta umefunga ndoa na kichaa akakuua! Lazima ujue hivi huyu mwanaume akikasirika huwa anafanyaje?Pengine akikasirika anapiga. Ukilijua hilo mapema unaweza kujipanga namna ya kudeal na mpigaji vinginevyo ingia kichwakichwa ufe! Siku hizi hata wanawake wanapiga! Tena wanapiga na kuua!
Kuna mwingine akichukia anawatafuta ma x wake wamtulize. Huoni kama hiyo ni hatari? Halafu ni hatari zaidi kama x wake yuko kwenye ndoa! Hapa haliwezi kusalia jiwe juu ya jiwe! Mwingine akichukia analala baa akinywa. Hapa unadhani mtajenga? Thubutu! Fanyeni uchunguzi wa akili vijana wangu kabla hamjajijia vitanzi!
Kosa la Tano
Tunaingia kwenye ndoa na wapenzi wa watu wengine. Yaani huyo mpenzi wako pengine alikuwa mpenzi wake, na huyu wake pengine alikuwa wako. Tumeponzwa na ubabe wa "Piga ua lazima nimpate yule mtoto" na kweli unampata. Pengine mtoto alikuwa na mpenzi wake aliyempenda kama samaki na maji kabla hajukutana na wewe Mr. Piga ua! Kwa sababu ya ushawishi wako wa piga ua, mtoto wa watu anamtema aliyempenda kwa dhati na kuangukia kwako. Kanuni za kupata mwenzi mwema zipo. Zifuateni. Muombe Mungu akupatie wako! Yupo! Fanya tu kuomba!
Kosa la Sita
Unaingia kwenye ndoa na mentality ya wanaume wote ni mbwa na wanawake wote wana akili za kitoto unategemea nini? Sikiliza ubaya hauna jinsia! Kuna wanaume wa hovyo lakini pia kuna wanawake wa hovyo sana. Hata hii lugha ya kwamba mwaume unaweza kumfanyia kila kitu lakini bado akachepuka ni ya hovyo pia.
Ulimuuliza kama hivyo ulivyomfanyia ndo anavitaka? Mtu anataka mchemsho wa kuku, wewe unaleta rost kila siku kwamba utazunguka bucha zote lakini nyama ni ileile. Hivi nyama ingekuwa ni ileile Yakobo angeteseka kumpata Rahel na wakati aliishapewa Lea? Hii imetufelisha sana ndiyo maana sitaki watarajiwa kuyarithi haya!
Kola la saba
Usawa wa kijinsia! Hapa napo kuna shida. Tena shida kubwa. Mnapeleka usawa hadi jikoni. Baba na mama sasa wote mnasubiri chakula mezani. Chakula kilichopikwa na dada. Baba akisifia chakula, mama ananuna! Hahahahaa!
Usawa wa kijinsia ndio umepelekea ongezeko la wanaume wengi kuwa wazembe. Wanataka walishwe. Yaani ulishwe na mtu anayebeba mimba yako miezi tisa na kunyonyesha mwaka mzima. Hapo huwezi kuwa salama. Sikiliza. Kwa mara ya kwanza Adamu alipokubali kulishwa na mwanamke ndio alifukuzwa Eden. Sisemi wanaume msilishwe. Nachosema Wanangu kabla ya kuingia kwenye ndoa mkasome vizuri hili somo la usawa wa kijinsia. Bila kulisoma na kulielewa tatizo la single mother halitaisha! Siku hizi hata mwanamke mwenye mimba anajiita single mother! Kumekucha!
Mwl. Denis Mpagaze
Muhenga wa Karne ya 21!
Karibu katika Jukwaa La Fikra tujenge nchi!
0 Comments