Tunaishi katika jamii ya ajabu kweli. Jamii ambayo kufikiri tofauti kunaweza kukuletea shida. 

Ukifikiri tofauti na baba yako utaambiwa umekua! Ukifikiri tofauti na mama yako ni dharau. 

Ukifikiri tofauti na viongozi wako wa chama utaambiwa umetumwa! Ukifikiri tofauti na walimu wako utaambiwa umeota mapembe! 

Ukifikiri tofauti na serikali yako utaambiwa umeanza uchochezi! Ukifikiri tofauti na wapiga kura wako utaambiwa umenunuliwa! 

Ukifikiri tofauti na mumeo utaambiwa unatoka nje ya ndoa! Ukifikiri tofauti na viongozi wako wa dini utatengwa! 

Ukifikiri tofauti na rafiki zako utaambiwa unaringa. Ukifikiri tofauti na mke wako utaambiwa unamnyanyasa kijinsia. Ukifikiri tofauti na ndugu zako watakwambia una roho mbaya.

 Kufikiri tofauti na bosi wako ni kuchoka kazi. Shida ni kufikiri tofauti. 

Kuhoji kwa nini kiongozi amekuwa kiranja kwa muda mrefu na wakati wenye sifa za kuongoza ni wengi ni kufikiri tofauti. 

Halafu kumbuka matokeo ya kufikiri tofauti na mfumo huwa siyo mazuri sana. Kuhoji kwa nini tunasema uchumi unakua na wakati mabenki yanafilisika ni uchochezi. “It is dangerous to be right when the government is wrong” alisema Mzee Voltaire mwanafalsafa wa Kifaransa aliyezaliwa mwaka 1694 na kufa 1778. 

Kufikiri hivyo ni sawa na kupiga konzi kwenye ncha ya mkuki. Kuhoji kwa nini hakuna nyongeza ya mshahara na wakati tumeambiwa uchumi unakua vizuri ni sawa na kutafuta nzi kwenye chakula. Wazee wa zamani wanasema mtu wa namna hiyo atakuwa ameshiba tu.

Usiache kufikiri tofauti, kufikiri tofauti ndiyo hutuongezea thamani.

Karibu katika Jukwaa la Fikra tufikiri tofauti kwa pamoja. 

Dady Lutelemla Jukwaani. 

WhatsApp namba 0620306815