Habari za wakati huu mpenzi msomaji wa Jukwaa la fikra, matumaini yangu ni kuwa unaendelea vyema na majukumu ya kujenga uchumi wa nchi. Hongera sana na Mungu akutangulie katika kila ukifanyacho kikanawiri na kuzaa matunda mengi.
Karibu Jukwaani,. Ndugu yangu Dunia ina maajabu mengi sana, ukiachilia mbali yale maajabu saba ya Ulimwengu yanayo fahamika kuna maajabu mengine makubwa ambayo yanashangaza kiasi kwamba yangetiliwa maanani yangekuwa kivutio kikubwa sana.
>Ajabu la kwanza, Watu wanataka wewe Uwe sahihi muda wote. Katika maajabu makubwa hili nalo linaweza kushika nafasi za juu sana, yaani siku zote watu huwa wanataka ni wewe tu ndiyo uwe sahihi wakati wao hawapo sahihi.
Yaani toka dunia iumbwe mtu anaweza kukwambia ni kosa la jinai kukaa chini halafu yeye muda wote anakaa chini.
*Hili nalo ni ajabu la Dunia.
>Ajabu la pili,. Hata mwizi naye anataka watu wasitarabu,. Je, unajua kuwa mwizi naye anaogopa kuibiwa? Unajua hilo? Kama haujui jitahidi ujue,. Kati ya watu wanaoongoza kufunga milango ya nyumba zao ni majambazi, mwizi ananunua kufuli la nini na anamuogopa nani kuja kumuibia wakati yeye ndiyo mwizi?
*Kama na hili una mashaka nalo kuwa kati ya maajabu ya Dunia, basi hata mashaka ana mashaka na wewe.
>Ajabu jingine ni pale Wanaume wanawaita wanawake ni malaya au kinyume chake, Yaani kwa akili ya kawaida utawaitaje wanawake malaya wakati huo umalaya wanafanya na Wanaume? Mbaya zaidi unawaita Wanaume malaya wakati wewe umewapanga hao hao wanaume kiasi kwamba ni wengi wanaweza kuanzisha darasa! Yaani inashangaza sana kuwaita wanawake malaya wakati wewe binafsi una vimada saba na point nne!
*Hii ni aibu inayoenda moja kwa moja kuwa ajabu la binadamu ambalo halionekani kwa macho.
>Ajabu lingine ni pale unapotaka kuolewa au kuoa mtu mwenye maadili mazuri. Unataka mtu aliye na maadili wakati wewe mwenyewe suala la maadili ni kitendawili!
Zamani watu waliolewa au kuoa kwa kuchimba historia ya familia, mzee anaingia field ya miaka mingi kukutafutia mchumba atakayekufaa kwa miaka yako yote hapa duniani,. Mazazi alikuwa na nguvu ya kuifelisha ndoa kwa vigezo vya mapungufu ya ukoo wenu haijarishi una umbo zuri kiasi gani.
*Leo maadili hayapo tena ila watu wamebaki kutafuta wenzi wenye maadili sijui watatoka wapi?
>Ajabu kubwa lingine ni pale unataka mkeo awahi kurudi nyumbani halafu wewe unarudi saa saba usiku kila siku na hutaki mtu akuulize kitu chochote, yaani kati ya jambo ambalo halihitaji maelezo ni hili, yaani mkeo akirudi saa mbili au saa tatu usiku inaweza ikawa mwisho wa mahusiano kabisa na wakati anayo sababu ya msingi. Kila siku wewe kurudi kwako ni umewahi sana ni saa sita usiku, na hautaki mtu aulize kuhusu hilo,. Na ikitokea ukaulizwa, basi nyumba itashuhudia Vita ya Urusi na Ukraine bila chenga.
*Hili ni ajabu kubwa sana la binadamu lisiloonekana kwa macho ambalo tunaweza kulifanya kama kivutio cha Dunia.
>Ajabu lingine la kiwango cha Dunia ni pale mtu mbahili anahitaji marafiki watoaji,. Suala la yeye kutoa ni maada kubwa mno lakini inapotokea kuhusu yeye kupokea hajali kabisa,. Usipompa utatangazwa kwenye kila televisheni na magazeti wakati yeye hataki kabisa kusikia habari ya utoaji.
Yaani huyu hata kanisani au msikitini hatoi sadaka lakini ni wa kwanza kuulizia kuhusu sadaka zilizotoka, nyumbani haachi kitu lakini ni wa kwanza kulalamika kuhusu njaa,..Halimi wala haendi shambani lakini ni wa kwanza kuulizia kuhusu mavuno.
*Je, bado unataka niendelee kuelezea kuhusu hili tu? Je, bado unahitaji tochi kumulika kuona kama hili nalo ni ajabu la binadamu? Jibu unalo mwenyewe Acha mimi nimalizie kisha nishuke Jukwaani.
>Ajabu lingine ni kuwa unaishi na watu ambao wanataka wewe Uwe serious wakati wao hawapo serious. Yaani katika maisha ya kila siku ni watu wangapi wanaokwambia kuwa haupo serious na wakati wao mambo wanayoyafanya ni aibu? Usinijibu ila tikisa kichwa tu.
Au ngoja nitoe mfano maana ni ajabu pia kuhubiri bila biblia,. Yaani mtu anakupigia simu kukuulizia kama watu washafika kwenye mkutano wakati yeye mwenyewe bado hajafika, na ukimwambia wamefika wawili tu anaanza kubwatuka,. Utasikia anasema "watu nao wamezidi kuchelewa yaani mpaka saa hizi ni wawili tu kweli" halafu anamaliza kwa kusema "wakiwa wengi kidogo uniambie sawa kaka". Anakata simu, mnaulizana huyu jamaa vipi?
Kama bado haujayaelewa maajabu haya ya binadamu nicheki kwa namba yangu ya WhatsApp +255620306815 au nipige kwa namba +255654836144.
Dady Lutelemla Jilasa, nashuka Jukwaani.
Share na watu maana kizuri kula na wenzako. Kibaya ni chako peke yako.
0 Comments