Ukiwasikiliza matajiri wote utasikia wanasema kama unafanya jambo kwa kutegemea kupata pesa umepotea, halafu maskini nao wanaamini. Hii nayo ni dhuluma iliyojificha! Sikiliza siku zote mshindi hawezi kukupa siri za ushindi kizembe!
Mikoa yote inalipa kodi lakini barabara nzuri na umeme wa uhakika vinapatikana mjini; tena kuna mikoa wameishakwangua barabara zaidi ya mara tano na kuweka mpya na wakati kuna maeneo wanakoishi wakulima tangu uhuru hawajaunganishwa kwa lami.
Unatupwa rumande kwa kesi ya kusingiziwa, kesi inaendeshwa weeeeeeeeeeee, mara unasikia Mkulu anasema hana interest ya kuendelea na kesi ifutwe, unaachiliwa na fidia ya kupokonywa haki ya kuwa huru bila kosa hupewi. Hii imekaaje watuhumiwa?
Waumini mnakabana koo kujenga shule ya kanisa kwa nguvu na michango yenu, lakini wakati wa kusoma wanasoma watoto wa matajiri maana maskini hawezi kulipa ada. Hii sijui watu wa Mungu mnaiona? Na kama mnaiona hebu semeneni nisikie!
Mwanafunzi akichelewa kulipa ada anazuiliwa kuingia darasani, masomo yanampita; siku akilipa ada analipia hadi zile siku ambazo hakusoma. Hii siyo dhuluma? Hapa siku ambazo hakuingia darasani asizilipie. Au unasemaje Mzee mwenzangu unayedaiwa ada?
Ukichelewa ndege unapigwa faini, lakini ndege ikichelewa haipigwi faini. Hapa ilitakiwa na ndege nazo zianze kupigwa faini maana zinabadilishaga ratiba hadi inakera. Hasa Afrika. Au unasemaje wewe mpanda ndege? Sisi usafiri wetu ni ule wa abiria chunga mzigo wako! Kule ndio hawajali muda kabisaaaa!
Mkulima akiuziwa mbegu feki anapewa mbegu nyingine yanaisha pasipokufidia mbolea iliyopotea shambani, nguvu aliyotumia shambani na muda wake. Hii siyo dhuluma? Nawauliza wakulima wenzangu maana maisha yenu nayajua.
Basi kama na wewe unaliona hili, tusaidiane kuamka pamoja.

0 Comments